C

C

Tuesday, April 29, 2014

STENDI UNITED YASIKILIZWA NA KAMATI YA NIDHAMU..

 

Kamati ya Nidhamu ya TFF imekubali malalamiko ya Stand United dhidi ya JKT Kanembwa kulalamikia timu hiyo kuchezesha wachezaji waliosajiliwa dirisha dogo kwenye mechi yao ya kiporo ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Mechi hiyo ya kundi C namba 22 awali ilichezwa mjini Shinyanga na kuvurugika, ambapo Bodi ya Ligi Kuu ya TFF iliagiza irudiwe kwenye uwanja huru, hivyo kuchezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
JKT Kanembwa ilishinda mechi hiyo iliyochezwa Februari 16 mwaka huu bao 1-0, lakini Stand United katika malalamiko yake ilidai timu hiyo ilichezesha wachezaji wanane waliosajiliwa katika usajili wa dirisha wakati mechi hiyo ilikuwa ni ya kiporo.
Kamati ya Nidhamu iliyokutana leo (Aprili 5 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Tarimba Abbas imeyakubali malalamiko hayo, hivyo kuipa Stand United ushindi wa pointi tatu na mabao mawili kwa mujibu wa Kanuni ya 8(22) ya FDL.
Upande wa walalamikiwa (JKT Kanembwa) uliowakilishwa na Mwenyekiti wake Luteni Menauri ulikiri kupokea maelekezo kutoka TFF kuwa wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo wasitumike katika mechi hiyo kwa vile ilikuwa ni ya kiporo.
Pia aliyekuwa Kamishna wa mechi hiyo Khalid Bitebo aliimbia Kamati kuwa baada ya kupokea maelekezo ya TFF alizifahamisha timu zote, lakini JKT Kanembwa iliondoa wachezaji wawili tu huku ikiwachezesha wengine wanane.
Nayo timu ya Gwasa Sports Club ya Dodoma iliyolalamika mbele ya Kamati hiyo kupingwa kunyang’anywa pointi sita na Kamati ya Mashindano ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) kwa kumchezesha mchezaji asiye halali kwenye Ligi ya Mkoa, malalamiko yake yametupwa.
Kamati imesema Gwasa imeshindwa kuonesha ushahidi kuwa ilimhamisha mchezaji huyo (Jeremiah Haule Jeremiah) kutoka timu ya AC Angry ya mjini Dodoma, na leseni iliyowasilishwa kuwa ndiyo aliyokuwa akiitumia AC Angry haoneshi msimu aliochezea timu hiyo.
Hivyo, Kamati ya Nidhamu imeridhia uamuzi wa Kamati ya DOREFA juu ya suala hilo ambapo Katibu wa Gwasa, Khalifa Ismail Ibrahim alikiri kuitwa kwenye kikao kilichofanya uamuzi huo na kuoneshwa vielelezo vilivyotolewa vya picha na fomu kuwa mchezaji huyo msimu wa 2013/2014 alichezea timu ya Katesh katika Ligi ya Mkoa wa Manyara.
Vilevile Kamati ya Nidhamu imebaini kuwa malalamiko ya Gwasa dhidi ya DOREFA hayakustahili kusikilizwa kwa vile kwa mujibu wa Kanuni, uamuzi uliofanywa dhidi yao haupaswi kukatiwa rufani.